Kulia ni Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas Gama. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Thabiti  Mwambungu.mwenye koti jeupe ni mganga mkuu wa Hospital hiyo Dkt Daniel Malekela Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,akimsalimia mtoto
NA STEPHANO MANGO,SONGEA

MADAKTARI na Wahudumu wa afya wanaofanya kazi katika Hospitali ya Rufaa mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiwa katika wakati mgumu baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, kuwajia juu na kukemea vitendo vya utoaji mimba ambavyo vimeshamiri katika hospitali hiyo.

Hali hiyo ilijitokeza katika ukumbi wa mikutano wa hospitali hiyo, ambapo Waziri Mkuu Majaliwa alimweleza Mganga mkuu, Daniel Malekela kwamba watumishi wake hasa madaktari wamekuwa na mazoea ya kufanya vitendo hivyo hasa kwa wanafunzi wanaosoma shule ya msingi na sekondari.

“Mganga Mkuu, hospitali yako inayosifa ya kutoa mimba, madaktari wamekuwa wakitumia wodi namba tano kufanyia kazi hii sasa natoa onyo kali ni marufuku kuanzia leo, sitaki kusikia tena jambo hili nitawafukuza kazi na kuwafunga”, alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Waziri Mkuu huyo alifafanua kuwa utoaji mimba, umekuwa ukifanyika hata katika jengo la upasuaji lililopo hospitalini hapo na kuongeza kuwa jambo hilo hataki kuliona linarudia tena na kwamba, hatakuwa na msamaha wowote kwa atakayehusika na kitendo hicho.

“Nyiee………… ole wenu, Mganga mkuu na Mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Ruvuma, hakikisheni hili jambo halijitokezi tena, likiendelea nitaanza kuwawajibisha ninyi”, alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu  huyo wakati alipokuwa ametembelea wodi za hospitali ya Rufaa ya mkoa huo, alijionea changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa majengo na malalamiko mbalimbali yaliyojitokeza kutoka kwa akina mama ambao walikuwa wakiuguza wagonjwa wao.

Akina mama hao kwa nyakati tofauti walimweleza kuwa wamekuwa wakikaripiwa na kutolewa lugha chafu, kutoka kwa baadhi ya waganga na madaktari wanaowahudumia jambo ambalo limekuwa kero kwao.

“Mmoja wa wagonjwa alimweleza Waziri Mkuu Majaliwa kwamba, “mimi binafsi hapa ninamgonjwa wangu amelazwa lakini naambiwa hakuna dawa nakwenda duka la dawa muhimu kununua ili mgonjwa wangu atibiwe, licha ya kununua dawa husika mganga wa zamu bado anataka nimpatie fedha ili ahudumie mgonjwa wangu je, hapo kuna haki”?, alihoji Rosemary Ngonyani.

Vilevile katika wodi ya watoto, walilalamikia kitendo cha watoto wao ambao ni wagonjwa kulazwa wawili wawili katika kitanda kimoja na kuiomba serikali iangalie kwa jicho la huruma tatizo hilo, ili liweze kupatiwa ufumbuzi.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza Katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma, Hassan Bendeyeko ahakikishe kuwa mkoa wake unatenga bajeti kwa ajili ya kupata fedha za kukarabati majengo ya hospitali hiyo ya rufaa na ujenzi wa majengo mengine mapya, ili kuweza kukidhi haja na kuondoka na kero ya kulala kitanda kimoja wagonjwa wawili.

Hata hivyo alitoa onyo kwa wanaotoa vifaa vya matibabu vya serikali na kuvipeleka kwenye zahanati, vituo vya afya au hospitali binafsi huku akijua kwamba ni kinyume na utaratibu atakayebainika atachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa kazi.
                      WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA AKITEMBEA NFRA RUVUMA
             MENEJA WA NFRA RUVUMA MORGAN MWAIPAYA AKIFAFANUA JAMBO

NA STEPHANO MANGO,SONGEA
WAZIRI Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hapa nchini, kuhakikisha kwamba wanajipanga kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wakulima wa zao la mahindi wanapatiwa magunia ya kuhifadhia zao hilo, katika maeneo ambayo yametengwa huko vijijini msimu ujao wa mavuno ya mazao ya chakula.

Agizo hilo amelitoa leo katika ziara yake ya siku tatu ya kutembelea na kuona maendeleo ya sekta mbalimbali mkoani Ruvuma, na kuhakikisha kwamba anatekeleza agizo la Rais John Magufuli linalosema hakuna Mtanzania atakayekufa njaa.

Alieleza kwamba, wafanyabiashara ambao wamekuwa wakipatiwa magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi na wakulima wanapojaribu kutafuta namna ya kuyapata magunia hayo, imekuwa ni tatizo kwao kuyapata kwa urahisi.

Vilevile Waziri Mkuu, Majaliwa alionesha kusikitishwa na vitendo hivyo vinavyofanywa na wafanyabiashara wajanja, ambao wamekuwa wakipita vijijini kuwarubuni wakulima na kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo hailingani na uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kuwa kumekuwa na mianya ya rushwa inayofanywa na wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Wakala huyo, kwa lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida akiendelea kuteseka na mazao yake shambani, jambo ambalo hivi sasa limekuwa ni kero kubwa hasa katika maeneo ambayo mazao ya chakula huzalishwa kwa wingi.

“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa ajili ya kuhifadhia zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba hayamfikii mkulima kule kijijini, badala yake yanaishia kwa watu wachache”, alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Vilevile alieleza kuwa serikali inawajibu wa kuhifadhi chakula katika mazingira yanayokubalika ili kisiweze kuharibiwa na wadudu waharibifu wa mazao, hivyo ameitaka Wakala wa hifadhi ya taifa ya chakula kanda ya Songea kuhakikisha kwamba mahindi yaliyohifadhiwa chini ya ardhi yanatafutiwa sehemu nyingine ya kuhifadhia ili yasiharibike.

Alifafanua kuwa uhifadhi wa nje wa zao hilo, usalama wake ni mdogo kwa asilimia 75 tu na kwamba mlundikano huo wa magunia yaliyosheheni mahindi katika hifadhi hiyo ya chakula unasababishwa na hifadhi kuwa na upungufu mkubwa wa maghala.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu Majaliwa alihoji juu ya msongamano wa magari aina ya malori yaliyopo kando kando ya barabara ya kutoka Songea kwenda Mbinga, huku akieleza kuwa hali hiyo imekuwa ikileta malalamiko mengi kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia NFRA kupakia mahindi, huwapatia watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu wengine kitendo ambacho kinaonyesha kuwa kuna upendeleo.

“Utaratibu unaotumika kuingiza malori hapa kwenu una malalamiko mengi, taarifa nilizonazo huingiza kwanza mtu anayejulikana, jambo hili likiendelea linaweza kuleta mtafaruku au matatizo yasiyokuwa ya lazima, nahitaji tatizo hili liwe mwisho na zingatieni haki na kupanga utaratibu mzuri”, alisisitiza.

Awali Mbunge wa Jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, Leonidas Gama alisema kuwa tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni kubwa hivyo ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya kutafuta masoko ili wakulima wadogo waweze kupata fursa ya kuuza mazao yao.

Gama alisisitiza kuwa ni vyema serikali irejeshe utaratibu wa awali, wa NFRA kununua mahindi vijijini kwa wakulima na kuachana na mfumo wa kuwatumia mawakala ambao hupita huko na kumkandamiza mkulima, kwa kununua mazao yao kwa bei ndogo.
   NA GIDEON MWAKANOSYA, MBINGA.

MFANYABIASHARA mmoja ambaye anajulikana kwa jina la Elias Mwalewela (46) anayeishi mtaa wa Manzese Mbinga mjini mkoani Ruvuma amekamatwa akitorosha kahawa ya maganda isiyokobolewa kiwandani kwenda Jijini Mbeya kwa njia ya magendo bila kufuata taratibu na sheria husika.

Aidha imeelezwa kuwa wakati zao hilo analitorosha, alikuwa akitokea wilayani Mbinga mkoani humo kwa lengo la kuipeleka huko, huku akijua fika kahawa ya maganda hairuhusiwi kusafirishwa kutoka wilaya moja kwenda nyingine.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Venance Mwamengo alisema kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema juu ya utoroshaji huo, alichukua jukumu la kufuatilia suala hilo ndipo baadaye alifanikiwa kumkamata katika kijiji cha Liganga wilaya ya Songea vijijini mkoani hapa kwa kushirikiana na askari aliokuwa nao.

Alifafanua kuwa alimkamata Disemba 30 mwaka jana, majira ya saa tano usiku akiwa na gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 818 ADH ambalo lilikuwa likiendeshwa na Geati Mwajungwa mkazi wa Lujewa Mbarali mkoani Mbeya.

“Huyu mfanyabiashara na dereva wake, baada ya kuwakamata niliwafikisha kituo kikuu cha Polisi wilaya ya Mbinga na gari lenye mzigo wa kahawa tani nne ambalo linashikiliwa hapo kituoni, hivi sasa wanaendelea kuhojiwa na taratibu zingine zitafuata ikiwemo kufikishwa Mahakamani au wanapaswa kulipa faini ya shilingi milioni 20”, alisema Mwamengo.

Mwamengo aliongeza kuwa watoroshaji hao walipofika mpakani mwa wilaya yake ambako kuna geti la ukaguzi wa mazao, walitorosha gari hilo likiwa na kahawa hiyo ndipo jitihada zilifanyika za kuwasaka na kufanikiwa kuwakamata katika kijiji hicho cha Liganga.

Alieleza kuwa wakati anawakamata, aliwakuta wakiwa na kibali cha usafirishaji kahawa safi (Clean Coffee) ambacho ni cha kampuni ya Tutunze Kahawa Limited, iliyopo wilayani humo ambayo inajishughulisha pia na ununuzi wa zao hilo.

Vilevile aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu husika, kibali hicho kinaruhusu kusafirishia kahawa iliyo safi tu, ambayo imekwisha kobolewa kiwandani na sio ya maganda kama walivyofanya watu hao.

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa wilaya ya Mbinga, Senyi Ngaga naye alithibitisha juu ya tukio hilo na kueleza kuwa mfanyabiashara huyo na dereva wa gari hilo wanahojiwa na Jeshi la Polisi wilayani humo, ili waweze kutolea maelezo ya kina juu ya kitendo hicho walichokifanya.

“Ni kweli taarifa nilizonazo wamekamatwa wakisafirisha kahawa ya maganda (Mbuni) na wapo Polisi wanahojiwa, wakimaliza kuhojiwa nitakuwa na taarifa kamili na kulitolea ufafanuzi mzuri jambo hili hapo baadaye”, alisema Ngaga.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tukio hilo alisema hataweza kutoa ufafanuzi wowote kuhusiana na jambo hilo, akidai kwamba ofisi yake bado halijamfikia.
 Image result for Said Mwambungu
NA STEPHANO MANGO,MADABA

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amewataka watendaji wa vijiji na kata wa mkoani humo kuhakikisha wanawafuatilia kikamilifu wanufaika wa mfuko wa maendeleo ya jamii Tasaf na kuwachukulia hatua wale wote ambao wametumia fedha hizo kinyume na malengo yaliyokusudiwa na
serikali.

Mwambungu aliyasema hayo jana wakati alipo kuwa akizindua baraza jipya la madiwani katika Halmashauli ya Madaba mkoani hapo ambayo imeanzishwa hivi karibuni na imekuwa na madiwani wa kata nane na vitimaalum wa tatu na mbunge na kufanya jumla ya madiwani 12.

Kwa mjibu wa mkuu huyo akitoa maagizo hayo alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya watu hasa akinababa kutumia vibaya fedha zinazotolewa naTasaf kwa madai kuwa serikali imewapatia watumie watakavyo jambo ambalo siyo kweli .

Alisema kuwa serikali imeamua kuziangalia kaya masikini ili
kuwanusuru na hali hiyo  lakini bado baadhi yao hawaoni jitihada
zinazofanywa na serikali na badala yake wamekuwa wakitumia misaada hiyo tofauti na malengo yaliyokusudiwa.

  “Nawaagiza watendaji kwa kuwa ninyi ndiyo mnaishi na kaya hizo na mnaziona zinavyotumia vibaya misaada hiyo hivyo ni vema mkazikamata na kuwaweka ndani ili iwe funzo kwa watu wengine ambao wanatumia vibaya kwa kujificha”alisema mkuu wa mkoa.

  Kwa upande wake mmoja aliyeteuliwa kushughulika na mambo ya Tasaf katika baadhi ya vijiji vya halmashauri ya Madaba  Vumilia Tawete akizungumza na gazeti hili kijijini hapo alisema kuwa kunabaadhi ya wanufaika bado hawana elimu ya kutosha kuhusiana na misaada hiyo hivyo ni vema kabla ya kuwagawia watalaam wauchumi watoe somo kwa walengwa namna ya matumizi ya fedha hizo.

Tawete alisema kuwa chamoto hizo tunakutana nazo kwa kuwaona baadhi yao hasa wakinababa akishapokea fedha anapitia moja kwa moja kwenye vilabu vya pombe huku wengine wakitoa maneno ya kejeli kuwa serikali imeamua kuwalipa mishara na watu ambao ni masikini.

Naye mbunge wa jimbo hilo Joseph Mhagama akimwelezea mkuu wa mkoa alisema kuwa licha ya maagizo ya kuwachukulia hatua watu hao lakini jimbo lake limejipanga vema kukabiliana na watumishi wazembe ambao wanafanya kazi kwa kutaka maslai.
 

Katika baraza hilo lilifanya uchaguzi ambao mgombea wa CCM  Vastus Mfikwa hakuwa na mpinzani hivyo alishinda kura zote 12 kwa kuwa halmashauri hiyo haina madiwani wa vyama vya upinzani huku mwenyekiti huyo akiahidi kufanya kazi za wananchi kwa kufuata kasi ya mheshimiwa
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr John Magufuli.
       MWISHO.
                   MKURUGENZI WA MADABA ROBART MAGENI
 
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
HALMASHAURI mpya ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma imejipanga kikamilifu kupima viwanja kwa ajiri ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Wilaya hiyo na viwanja vya makazi ya wananchi kwa kufuata taratibu za mipango miji na kuufanya mji huo kuwa wa kisasa zaidi

Akizungumza na gazeti hili jana Ofisini kwake Afisa Ardhi wa Halmashauri hiyo Leonsi Mtalemwa  alisema kuwa halmashauri inatarajia kuanza mchakato wa ujenzi wa nyumba za watumishi na kwa kuanzia mpango huo utaanza na ujenzi wa nyumba za wakuu wa idara ambao wanastahili kupewa nyumba za kuishi katika utumishi wao

Mtalemwa alisema kuwa tayari viwanja 600 vimeshapimwa likiwemo stendi ya mabasi ambapo wananchi waliopewa viwanja katika eneo hilo wametakiwa kukamilisha ujenzi wa vibanda vya biashara kama mpango ulivyowekwa na kufanya matumizi bora ya ardhi yanatekelezwa

Alisema kuwa kuna eneo jingine ambalo linatakiwa lipimwe viwanja bado halijalipwa fidia hivyo jitihada zinaendelea ili kupata fedha na kulipa fidia ili upimaji  wa viwanja uendelee kwa ajiri ya ujenzi wa makao makuu ya Hakmashauri, viwanja kwa ajiri ya ujenzi wa nyumba mbalimbali na maeneo ya kuabudia na kuzikana

Naye Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Prosper Luambano alisema kuwa kwasasa Halmashauri inakarabati jengo la kituo cha habari kwa wakulima ili kuwezesha ofisi ya watumishi wa kada mbalimbali kuanzia kazi zao hapo wakati hatua zingine za ujenzi wa ofisi za kutumu zikiendelea

Luambano alisema kuwa Halmashauri imepeleka ombi maalum Hazina ili kuwezesha upatikanaji wa gari la Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya,ujenzi wa nyumba yake pamoja na upatikanaji wa umeme na maji kwenye makazi ya mkurugenzi huyo

Alisema kuwa Halmashauri hiyo inatarajia kuanza mchakato wa ujenzi wa jengo la makao makuu yake ambalo linatarajiwa kujengwa kwenye maeneo mapya yatakayopimwa vizuri upande wa barabara ya Songea-Njombe ambapo maombi ya mpango huo mahsusi umejumlishwa kwenye mpango wa bajeti wa Halmashauri kwa mwaka 2016/17 na kuendelea hadi ujenzi utakapokamilika
        WAENDESHA BODA WAKIWA KWENYE KIJIWE CHAO CHA KUSAKA ABIRIA
Na Julius Konala,Songea

ZAIDI ya waendesha bodaboda 100 wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wamejiunga na mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii(NSSF) mkoani Ruvuma.

Hayo yalisemwa jana na Meneja wa mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii wa mkoa wa Ruvuma Dominic Mbwette,wakati alipokuwa akiongea na gazeti hili ofisini kwake mjini Songea.

Mbwette alisema kuwa shirika lake limeamua kuendesha semina ya siku moja kwa waendesha bodaboda hao ili waweze kujiunga na mfuko wa mafao ya matibabu na kuumia kazini kwa kuwa wao ndio wahanga wakubwa.

Alisema kuwa kiingilio kwa ajili ya mfuko huo ni shilingi 20,000 ambazo zitasaidia kuwawezesha kutibiwa katika hospitali mbalimbali hapa nchini huku akidai kuwa shirika hilo linatarajia kuwafikia waendesha bodaboda wa wilaya ya Namtumbo,Songea,Madaba,Tunduru na Nyasa.

Meneja huyo pia amewaomba wajasiriamali mbalimbali wakiwemo wakulima kujiunga na mfuko huo wa  NSSF  ili waweze kupata mafao mbalimbali ya matibabu,mafao ya uzazi,mafao ya kuumia kazini na msaadawa mazishi ili iweze kuwasaidia pindi wanapopatwa na matatizo.

Alisema kuwa tayari shirika lake limekwisha toa elimu hiyo kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Udaktari cha st.Augustine Peramiho,waendesha bodaboda na kundi la jumuia ya umoja wa wanawake wa CCM mjini Songea.

Kwa upande wao baadhi ya waendesha bodaboda hao wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti walisema kuwa wameamua kujiunga na mfuko huo baada ya kuona kuwa wao ndio wahanga wakubwa wa kupata ajali bila ya kuwa na msaada wowote wa matibabu.